Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imetoa wito kwa Watumishi wote wa Umma walio katika Taasisi na Mashirika ya Umma kote nchini, kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Msajili wa Hazina, Lightness Mauki, amesema Watumishi wa Umma wana nafasi ya kipekee katika kuhakikisha dira ya maendeleo ya Taifa inatimia, kwa kuwa wao ndio watendaji wakuu wa Sera na mipango ya Serikali.
Mauki amesisitiza kuwa ushiriki wa watumishi wa Umma ni sehemu muhimu ya kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji na amani ya Nchi, pamoja na nguzo kuu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati wa juu unaokadiriwa kufikia dola za Kimarekani Trilioni 1 ifikapo mwaka 2050.

“Ushiriki wa watumishi wa Umma katika uchaguzi ni zaidi ya kutekeleza haki ya kikatiba.
Ni tendo la kizalendo linaloimarisha misingi ya utawala bora na kuonesha dhamira ya dhati ya kujenga Tanzania yenye maendeleo jumuishi na uchumi imara,” amesema Mauki.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka dira thabiti ya maendeleo inayolenga kujenga uchumi shindani na jumuishi unaotegemea uwazi, uadilifu na ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya Taifa.
Aidha amesema kupiga kura ni wajibu wa kiraia unaoimarisha umoja, uthabiti wa Taifa na uwajibikaji, na kwamba Kupiga kura kunawawezesha wananchi wakiwemo watumishi wa umma kuchagua viongozi wenye maono, uadilifu na uwajibikaji, ambao watasimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa tija.