Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa serikali imetangaza siku hiyo kuwa ya mapumziko ili kutoa fursa kwa kila mwenye sifa kutimiza haki yake ya kikatiba ya kupiga kura.
Akihutubia maelfu ya wananchi wa Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mkuu, Dkt. Samia amesema maandalizi yote yamekamilika huku vyombo vya ulinzi na usalama vikihakikisha kuwepo kwa mazingira salama na yenye amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Aidha, amewapongeza Watanzania kwa kufanya kampeni za kistaarabu, zenye hoja na zisizo na matusi, akisema mwenendo huo unaonesha ukomavu wa kisiasa na kuheshimiana miongoni mwa vyama vyote vya siasa.

Dkt. Samia amewataka viongozi wa vyama vyote kuwa na utulivu na kuruhusu wananchi kufanya maamuzi yao kwa uhuru, huku akiwahimiza Watanzania wote kutumia haki yao ya kupiga kura ili kuimarisha demokrasia nchini.
Ametoa wito maalum kwa wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha ushindi wa heshima kwa chama hicho.
“Hakuna upinzani dhaifu wala upinzani mwepesi, twendeni kwa nguvu zote tukachague wagombea wa CCM, twendeni tukachague kazi na utu, twendeni tukachague CCM,” amesisitiza Dkt. Samia.