Jeshi la Polisi nchini limesema hali ya usalama inaendelea kuwa shwari kote nchini kuelekea siku ya kupiga kura kesho, Oktoba 29, 2025, na limewahakikishia Watanzania wote kuwa hakuna tishio lolote la kiusalama lililobainika hadi sasa.
Akizungumza leo October 28, 2025 jijini Dodoma, Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, amesema jeshi limejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wanatekeleza haki yao ya kupiga kura katika mazingira ya amani, utulivu na usalama wa kutosha.
Ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, kumekuwa na juhudi za baadhi ya watu wachache wanaojaribu kuvuruga amani kwa njia za kidijitali baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa vitendo, jambo ambalo jeshi limeanza kulifuatilia kwa karibu.
Kwa mujibu wa Polisi, baadhi ya watu hao wamekuwa wakitumia matukio ya video na picha yaliyowahi kurekodiwa katika nchi nyingine, kisha kuyahariri kwa kuweka sauti zenye lafudhi ya Kiswahili ili kuonekana kama ni matukio yanayotokea Tanzania, kwa lengo la kupandikiza hofu na taharuki kwa wananchi.
Aidha, Jeshi hilo limebainisha kuwa wapo pia watu waliopangwa kutoa taarifa zenye maneno ya uchochezi na tungo tata zinazolenga kuchafua taswira ya taifa, huku wengine wakichapisha picha za viongozi wakuu na kuziwekea maneno au sauti za uongo.
Jeshi la Polisi limeongeza kuwa linaendelea kuwafuatilia na kuwakamata wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa mujibu wa sheria, likiwataka wananchi wasishiriki kusambaza taarifa hizo, kwani ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao.