Kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Mwanaharakati Mange Kimambi imeahirishwa mpaka Januari 28, 2026 baada ya Jamhuri kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Shauri hilo Leo limeitwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hassan Makube ambapo upande wa Jamhuri umeieleza mahakama kuwa upelelezi bado na uomba shauri kupangiwa tarehe nyingine.
Upande wa Mange Kimambi haukuwa na Wakili wa utetezi hivyo Hakimu Makube akaagiza upande wa Jamhuri kukamilisha taratibu zote ili januari 28 shauri lianze kusikilizwa.
Kimambi anakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kiasi cha Shilingi milioni Sh138.5 ambapo kati ya Machi 1 na Machi 31, 2022, maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, akifahamu kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu.
Inadaiwa pia alizipata fedha hizo kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kibali na kuzidai kwa vitisho.
Hatua hiyo mpya inakuja mwezi mmoja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari, kueleza kuwa ofisi yake inaangalia uwezekano wa kumchukulia hatua kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano.