Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo, ameiagiza Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kuongeza kasi ya kupanga na kupima ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwamo miradi ya kilimo, makazi na uwekezaji, ili kupunguza migogoro na kuweka msingi imara wa maendeleo endelevu.
Akizungumza leo Desemba 17, 2025, wakati wa kufungua kikao kazi cha Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kilichofanyika makao makuu ya wizara hiyo jijini Dodoma, Dk Akwilapo amesisitiza umuhimu wa kukuza matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa takwimu za ardhi na mipango.

Amesema Tanzania inaendelea kukabiliwa na changamoto za matumizi ya ardhi, zikiwamo za migongano kati ya shughuli za kilimo na ufugaji, malisho na uhifadhi pamoja na upungufu wa maeneo ya uwekezaji wa kimkakati unaosababishwa na mabadiliko ya matumizi ya ardhi yasiyopangwa.Changamoto nyingine alizozitaja ni uharibifu wa mazingira unaotokana na uvamizi wa vyanzo vya maji, ukataji miti hovyo, matumizi yasiyo rasmi ya ardhi, athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ukuaji wa kasi wa miji unaohitaji mipango bunifu na matumizi bora ya ardhi.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Dk Akwilapo amesema Serikali inategemea utaalamu na ushauri wa Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ili kuhakikisha ardhi inatumika kwa tija, usawa, usalama na uendelevu, huku akiiagiza Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kuisaidia kamati hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anthony Sanga amesema migogoro ya wakulima na wafugaji imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma kutokana na juhudi za tume.
