Serikali imesema ipo katika maandalizi ya kusajili watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 ili kuwapatia namba ya utambulisho wa kipekee (Jamii Namba) itakayotumika kuanzia kuzaliwa hadi mwisho wa maisha ya mtu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene leo December 19, 2025, wakati wa ziara ya kukagua uzalishaji wa vitambulisho katika Kituo cha Kuchakata Taarifa cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Waziri Simbachawene amesema zoezi hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Agosti 10, 2023, ambapo jumla ya shilingi bilioni 11.3 zimetengwa kwa ajili ya usajili wa watoto ambapo wilaya za majaribio ni Kilolo, Kusini Unguja na Rungwe.
Waziri Simbachawene ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi waliokwisha andikishwa kufika kwenye vituo walivyojiandikisha ili kuchukua vitambulisho vyao.
“Jamii namba itakayowatambua watoto ni jambo kubwa linalokuja.
Itapunguza malalamiko mengi kwa sababu mtu atatambulika tangu anapozaliwa,” amesema Waziri Simbachawene.
Aidha, Waziri Simbachawene amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wananchi waliotumia taarifa zisizo sahihi za utambulisho, wakiwemo walowezi, wakimbizi au waliotumia majina yasiyo yao, ili wajitokeze kusahihisha taarifa zao na kuepuka matatizo ya baadaye ikiwemo kukosa ajira au uraia.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Omar Mmanga, amesema mamlaka hiyo inaendelea na usajili wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora), ambapo hadi sasa Watanzania 1,465 wameshatambuliwa na kuandikishwa.
Amesema jumla ya vitambulisho 21,245,975 tayari vimezalishwa nchini, lengo likiwa ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na utambulisho popote alipo.