Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Profesa Mohamed Janabi amezitaka nchi za Afrika kuongeza fedha katika bajeti zao za afya, ili kupambana na kupungua kwa misaada ya rasilimali fedha.
Amesema hiyo imetokana na kujitoa kwa mataifa makubwa ikiwemo Marekani, hali iliyosababisha kupungua kwa asilimia 70 ya rasilimali fedha.
Profesa Janabi ameyasema hayo leo Desemba 22, 2025 wakati WHO kupitia Ofisi yake ya Kanda ya Afrika (WHO-AFRO) ilipokuwa ikisaini Hati ya Makubaliano (MoU), kuimarisha ushirikiano wa kikanda wa afya na Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC) katika Ofisi za WHO Tanzania.
Amesema asilimia kubwa ya milipuko inatokea katika nchi za Afrika, na katika kuishughulikia inahitaji rasilimali fedha nyingi, lakini mdau mkubwa aliyefadhili amejitoa, hivyo kupunguza misaada kwa kiwango kikubwa.
“Misaada imepungua kwa asilimia 70, kilichobaki sasa nchi zinatakiwa kujipanga upya katika kujisaidia kwa kutenga bajeti kubwa za afya ili kuwa na uwezo wa kushughulikia changamoto hizi pindi zinapojitokeza,” amesema.
Amesema kupungua kwa misaada hiyo pia ilichangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa rasilimali watu kwa asilimia 25, na hivyo wataalamu wengi wenye ujuzi mkubwa waliondoka.