
Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 277 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kugharamia huduma mbalimbali za Virusi Vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI nchini, ili kupunguza utegemezi kwa wafadhili wa kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Samwel Sumba, alipokuwa akizungumza katika Maonesho ya 32 ya Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Dkt. Sumba amesema kuwa uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya dhati ya kuimarisha afua za VVU na UKIMWI kwa kutumia rasilimali za ndani, hatua inayolenga kupunguza maambukizi mapya na kuboresha maisha ya watu wanaoishi na virusi hivyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Athari za UKIMWI ya mwaka 2022/2023, Tanzania kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi ni asilimia 4.4, ambapo wanawake wanaongoza kwa asilimia 5.6, ikilinganishwa na wanaume wenye asilimia 3.0.