Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mhandisi Chacha Wambura, amewataka maafisa usafirishaji maarufu kwa jina la bodaboda kuwa mabalozi wa kutunza amani na utulivu wa nchi, na kujiepusha kushiriki katika vitendo vinavyohatarisha uvunjifu wa amani.
Mhandisi Chacha ametoa wito huo wakati wa kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo waendesha bodaboda 2,000, pamoja na mafunzo ya usalama barabarani, yaliyofadhiliwa na mbunge huyo. Amesema baada ya kukamilisha mafunzo hayo, washiriki watapatiwa leseni za udereva.
Amesema waendesha bodaboda wana wajibu mkubwa wa kulinda amani ya nchi na kuzingatia sheria, kwa kuwa wao ni sehemu muhimu ya jamii na wanakutana na wananchi wengi kila siku katika shughuli zao za usafirishaji.
Hata hivyo Mbunge huyo amekabidhi mfano wa hundi ya Shilingi milioni saba kwa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Chato, ikiwa ni mchango wake katika kugharamia mafunzo na leseni kwa vijana hao, ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na kwa usalama zaidi.
