
Bondia Juma Choki ameingia hatua ya 16 bora baada ya kushinda pambano lake dhidi ya bondia wa Ufilipino Bryx Piala katika mashindano ya ngumi ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Saudia Arabia.
Choki alishinda kwa pointi za majaji watatu yaani 58-56, 59-55 na 59-55 katika pambano la hatua ya 32 bora.
Kwa ushindi huo, Choki atakutana na bondia wa Mexico Hector Munguia ambaye yeye ametinga hatua hiyo baada ya kumchapa Idris Gbadamosi kwa TKO raundi ya sita.
Hector mwenye nyota tatu na nusu ana rekodi ya kushinda mapambano 15 akitoka sare pambano moja na hajapoteza.
Washindi wanne wa uzito Featherweight, Super Lightweight, Middleweight na Heavyweight wataondoka na Dola za Marekani 200,000 sawa na zaidi ya Milioni 500 za Tanzania.