Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amewaonya wananchi wanaozifunga fedha kama shada la maua kwa ajili ya zawadi kwa wapendwa wao, hususan katika kipindi hiki cha msimu wa Sikukuu ya Wapendanao (Valentine).
Gavana Tutuba amesema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria na husababisha uharibifu wa fedha, akisisitiza kuwa fedha ni tunu ya Taifa, na utaratibu wa kuziweka katika mashada ya maua mara nyingi huhusisha kubandikwa kwa gundi pamoja na kukunjwa, hali inayochangia kuchakaa kwa haraka au kuchanika.
Aidha, Gavana Tutuba amesisitiza kuwa kutokana na uharibifu huo, Benki Kuu hulazimika kuchapisha fedha mpya mara kwa mara, jambo linaloongeza gharama kwa Taifa hivyo kila anayeshika fedha ya Tanzania ana wajibu wa kuzitunza na kuzihifadhi, kwa kuwa ni miongoni mwa alama na tunu muhimu za Taifa
