Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeingilia soko la kubadilisha fedha za kigeni baina ya benki (IFEM) kwa kuuza dola za Marekani ili kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni nchini.
Katika taarifa kuhusu mnada huo iliyotolewa na BoT imeuza jumla ya dola za Marekani milioni 15.75 kwa benki za biashara kwa wastani wa shilingi 2,572.56 kwa dola moja.
Jumla ya benki 30 zimeshiriki katika mnada huo wa dola, ambapo benki 18 zimefanikiwa kununua fedha hizo.
Ushiriki huo unaonesha umuhimu wa hatua ya BoT katika kusaidia mzunguko wa fedha za kigeni, hususani kwa sekta zinazotegemea uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.
Hatua ya BoT inatarajiwa kusaidia kupunguza presha ya upungufu wa dola nchini na kuleta unafuu kwa biashara na wananchi wanaotegemea miamala ya fedha za kigeni.
