Staa wa Pop, Britney Spears, anaripotiwa kuuza haki za catalogue yake yote ya muziki katika mkataba unaokadiriwa kufikia dola milioni 200 kwa mujibu wa vyombo vya habari.
Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 44 anasemekana kukamilisha makubaliano hayo tarehe 30 Desemba na kampuni huru ya uchapishaji wa muziki Primary Wave. Hata hivyo, thamani halisi ya mkataba huo haijatangazwa rasmi.
Spears ni mmoja wa wasanii wa kike waliouza nakala nyingi zaidi duniani. Alipata umaarufu wa kimataifa mwishoni mwa miaka ya 1990 kupitia nyimbo maarufu kama “…Baby One More Time,” “Oops!… I Did It Again,” “Toxic,” na “Gimme More.”
Tangu kuanza kwake mwaka 1999, ametoa albamu tisa za studio na kuuza zaidi ya nakala milioni 150 duniani kote. Pia ameshinda tuzo mbalimbali ikiwemo Grammy.
Mnamo Januari 2024, Spears alitangaza kuwa “hatarudi tena katika tasnia ya muziki huku mradi wake wa mwisho wa muziki ulikuwa duet ya mwaka 2022 na gwiji wa muziki wa Uingereza Elton John.
Kampuni ya Primary Wave, iliyoanzishwa na Lawrence Mestel, imejijengea sifa kwa kununua haki za catalogue za wasanii wakubwa. Tayari imepata haki zinazohusiana na mali za wasanii kama The Notorious B.I.G., Prince, na Whitney Houston.
Spears anaungana na orodha ya wasanii wakubwa waliouza catalogue zao hivi karibuni.
Mwaka 2023, Justin Bieber alifunga mkataba wa dola milioni 200. Wasanii wengine kama Justin Timberlake na Shakira pia wamefanya makubaliano kama hayo.
