
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, akibainisha kuwa lishe ni moja ya nguzo muhimu katika mafanikio ya kielimu kwa watoto.
Akizungumza Alhamisi ya Mei 15, 2025, katika mdahalo wa Wiki ya Ubunifu unaofanyika jijini Dar es Salaam ukihusisha mawaziri mbalimbali Profesa Mkenda amesema uchunguzi wa wizara umebaini kuwa chakula shuleni ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma na kiafya.
Amesisitiza kuwa licha ya elimu kutolewa bila malipo, wazazi wanabaki na jukumu la kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji mengine muhimu kama sare, vitabu na chakula.
Hata hivyo, amekiri kuwa uwezo mdogo wa kiuchumi kwa baadhi ya familia umekuwa ukiathiri utekelezaji wa jukumu hilo.