Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amefafanua kuwa nchi inapokuwa na akiba ya mafuta ya miezi mitatu, haimaanishi mafuta hayo yote yamehifadhiwa kwenye matenki ya ndani pekee.
Akiba hiyo ni mjumuisho wa mafuta yaliyopo kwenye maghala (depo), yale yaliyopo bandarini yakishushwa, mafuta yaliyo njiani kwenye meli, na kiasi kilichohakikishwa kupitia mikataba ya ununuzi na kampuni za usambazaji.
Chalamila ameongeza kuwa bei ya mafuta nchini hupangwa kulingana na gharama za ununuzi katika soko la dunia kwa utaratibu wa mwezi uliopita (M-1).
Hii ina maana kuwa mafuta yanayouzwa mwezi Aprili yanazingatia bei ya soko la dunia ya mwezi Machi. Hivyo, mabadiliko yoyote ya bei duniani, kama yale yanayosababishwa na vita, huchelewa kuonekana kwenye pampu kwa mwezi mmoja.
Katika maelezo yake, Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa kiasi hiki cha mafuta ni mchanganyiko wa bidhaa iliyopo na mipango ya kisheria inayohakikisha nchi inabaki na nishati ya kutosha.
Utaratibu huu unahakikisha kuwa nchi inakuwa na nishati ya uhakika huku bei ikiongozwa na uhalisia wa gharama za ununuzi zilizofanyika katika soko la kimataifa.
