Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza maandalizi ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu utakaotekelezwa kikamilifu kuanzia mwaka 2028, ambao utaanzisha elimu ya lazima kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Chini ya mfumo huo, shule ya msingi itakuwa na madarasa sita na sekondari madarasa manne, jumla ikiwa madarasa 10.
Amesema utekelezaji wa mtaala huo utaanza kwa majaribio Januari 2027 katika madarasa ya sita na saba kabla ya kuanza rasmi mwaka 2028.
Akizungumza na wananchi wa Mabogini, wilayani Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, leo Februari 20, 2026, Waziri Mkuu amehimiza vijiji kutenga maeneo toshelevu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya na kuongeza vyumba pale ambapo vilivyopo havitoshelezi, ili kuepusha gharama za kubomoa na kujenga upya baadaye.
Akiwa katika eneo hilo Mabogini, Waziri Mkuu amepokea pia mapendekezo ya wananchi ikiwemo ujenzi wa shule, barabara za lami na madaraja.
Kuhusu barabara, ameelekeza mradi uanze kwa kiwango cha kupitika mara moja huku juhudi zikifanyika kuifikisha katika kiwango cha lami haraka iwezekanavyo.
Amesema barabara hiyo itasaidia utoaji wa huduma za kijamii na kukuza maendeleo ya kiuchumi, ikiwemo kutumika kama barabara mbadala (bypass).
