
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amezitaka hospitali zote nchini kuhakikisha zinasimamia na kulinda miundombinu iliyowekezwa na Serikali.
Akizungumza jana alipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, Mhagama amesema Serikali tayari imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 19.8 katika hospitali hiyo kati ya Shilingi bilioni 29 zilizotolewa kitaifa, hivyo ni wajibu wa watumishi kulinda miundombinu hiyo kwa wivu mkubwa.
Aidha, amewataka watumishi wa sekta ya afya kuzingatia maadili ya kazi, kukataa vitendo vya ukiukwaji wa kiapo cha taaluma.
Amesisitiza pia umuhimu wa idara ya Tehama kuboresha usimamizi wa hospitali na kutokomeza mapungufu yaliyopo.
Pia amesisitiza elimu ya lishe kwa kina mama ili kupunguza vifo vya watoto vinavyotokana na utapiamlo.