Uongozi wa jeshi la taifa nchini DRC umelaani mashambulizi yaliyofanywa jana Desemba 2 2025 na kundi la waasi wa M23 kwenye ngome za jeshi katika mkoa wa Kivu kusini na kusababisha maafa mengi.
Msemaji wa jeshi la taifa nchini DRC Jenerali Sylvain Ekenge amesema kuwa M23 wakisaidiwa na jeshi la Rwanda wameshambulia miji ya Katogota, Lubarika na Kaziba, hali inayokiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa nchini Qatar.
Mashambulizi hayo yanafanyika wakati Rwanda na DRC zikitarajia kuelekea Washington Marekani kusaini mkataba wa amani mashariki mwa nchi hiyo.
Mpango wa Kusaini mkataba kati ya nchi hizo ukiwa unaendelea waasi wa M23 na jeshi la Rwanda bado wanazidisha mashambulizi na kusababisha vifo vya raia na wengine kuyakimbia makazi.
Aidha Jenerali Ekenge amepongeza jeshi la taifa na wazalendo kwa ujasiri wa kufurusha waasi hao na kudhibiti miji waliyokuwa wamevamia, na amewataka raia wa Uvira na Kaziba kuwa watulivu wakati jeshi likijaribu kurejesha usalama.