
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mabadiliko muhimu ya Katiba yake ya Januari 1977, kwa lengo la kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya uendeshaji wa chama.
Mabadiliko hayo yamepitishwa rasmi Mei 29, 2025 katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika jijini Dodoma, yakilenga kuboresha mifumo ya utendaji na usimamizi wa rasilimali za chama.
Miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuingizwa rasmi kwa utaratibu wa mikutano ya mtandao (E-Meeting) katika Katiba ya chama, kwa ngazi zote kuanzia wilaya hadi Mkutano Mkuu wa Taifa.
Lengo kuu ni kurahisisha utendaji, kuongeza ufanisi, na kupunguza gharama, hususani katika nyakati za dharura.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa chama kimeamua kuendana na kasi ya dunia ya kidijitali ili kuboresha mifumo ya mawasiliano na uendeshaji wa shughuli zake.