
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, leo Alhamisi, Juni 26, 2025 inatarajiwa kutoa hukumu za mashauri mawili yaliyofunguliwa na raia wa Tanzania – wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani, wagombea na wapiga kura dhidi ya Serikali ya Tanzania.
Shauri la kwanza lilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu na wenzake na la pili lilifunguliwa na Kiongozi wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Abdul Nondo na wenzake wawili – Deusdedith Rweyemamu na Paul Kaunda.
Katika mashauri hayo wadai wanaishtaki Serikali ya Tanzania wakidai ilihusika na vitendo mbalimbali vilivyokiuka haki zao za kiraia na kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Hukumu za mashauri hayo zimepangwa kusomwa leo saa 4:00 asubuhi, huku mwenendo huo ukirushwa moja kwa moja kwa njia ya mtandao kupitia kiungo cha Mahakama hiyo.
Katika kesi ya Shaibu na wenzake waliiomba Mahakama kushughulikia ukiukwaji wa jumla wa haki za binadamu za kiraia na za kisiasa uliofanywa na Serikali wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020.