Pedro Goncalves, Kocha Mkuu wa Yanga SC, amesema kuwa mchezaji Dickson Job ameumia na anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili, ingawa muda huo unaweza kubadilika kulingana na maendeleo ya hali yake. Kuhusu Pacome, kocha huyo amesema bado hajawa fiti kwa asilimia mia moja na wataendelea kufuatilia hali yake baada ya mazoezi ya leo.

Kocha Goncalves amekiri kuwa kikosi chake kinakabiliwa na changamoto ya kuwa na idadi kubwa ya majeruhi kwa sasa. Hata hivyo, amesisitiza kuwa hali hiyo haitawazuia wachezaji waliopo kujituma kwa nguvu zote katika maandalizi na mchezo ujao.
Yanga inaelekea katika mchezo wa kesho dhidi ya Singida Big Stars ikiwa na presha ya kupata matokeo mazuri, licha ya changamoto ya majeraha kwa baadhi ya nyota wake muhimu.
Nahodha msaidizi wa Yanga alipata majeraha hayo katika mchezo wa Kariakoo Derby dhidi ya Simba SC, uliopigwa kwenye dimba la New Amaan Complex, visiwani Zanzibar Jumapili.
