
Siku ya Kimataifa ya Familia (IDF) huadhimishwa tarehe 15 Mei 2025 inatoa mwanga kuhusu umuhimu wa sera za familia katika kufikia maendeleo endelevu. Kwa mwaka huu, maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Sera za Familia kwa Maendeleo Endelevu,
Kauli mbiu hii inalenga kuonyesha mchango wa familia katika utekelezaji wa Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu ikiwa ni kuelekea Mkutano wa Pili wa Dunia kuhusu Maendeleo ya Jamii.
Sera za Familia na Mkutano wa Pili wa Dunia kuhusu Maendeleo ya Jamii
Mkutano wa Pili wa Dunia kuhusu Maendeleo ya Jamii, utakaofanyika Doha, Qatar kuanzia tarehe 4 hadi 6 Novemba 2025, utatoa fursa muhimu kwa nchi duniani kuimarisha ahadi za kupambana na umasikini, kuhakikisha kazi bora, na kuongeza ujumuishaji wa kijamii.
Mkutano huu utajikita katika masuala yaliyoainishwa kwenye Azimio la Copenhagen la mwaka 1995, ambalo lilitambua familia kama nguzo muhimu katika jamii na kusisitiza umuhimu wa uwiano kati ya kazi na familia pamoja na usawa wa ushirikiano ndani ya kaya.
Siku ya Familia ya mwaka 2025 itasisitiza umuhimu wa kuingiza sera zinazozingatia familia katika mipango ya maendeleo ya kitaifa ili kukabiliana na changamoto kubwa za kisasa kama vile mageuzi ya kiteknolojia, mabadiliko ya idadi ya watu, miji, uhamiaji, na mabadiliko ya tabia nchi.
Historia ya Siku ya Familia
Umoja wa Mataifa ulianza kuzingatia masuala ya familia katika miaka ya 1980. Mwaka 1983, Baraza la Kiuchumi na Kijamii lilipendekeza kuanzishwa kwa juhudi za kuongeza uelewa kuhusu changamoto na mahitaji ya familia.
Katika mkutano wa mwaka 1985, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulijadili masuala ya familia na kuanzisha mchakato wa kutangaza mwaka wa kimataifa wa familia, ambao ulizaa Azimio la Desemba 1989, linalotangaza mwaka wa Kimataifa wa Familia.
Mwaka 1993, Mkutano Mkuu ulipitisha azimio likitangaza tarehe 15 Mei ya kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Familia. Siku hii hutumika kama fursa ya kuhamasisha uelewa kuhusu masuala yanayohusiana na familia na kuongezea ufahamu wa michakato ya kijamii, kiuchumi, na demografia inayozigusa familia.
Malengo ya Maendeleo Endelevu na Familia
Mnamo tarehe 25 Septemba 2015, nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilipitisha kwa kauli moja Malengo ya Maendeleo Endelevu, ambayo ni seti ya malengo 17 inayo lengo la kumaliza umasikini, kuboresha hali ya kijamii, na kulinda mazingira.
Familia na sera zinazozingatia familia ni sehemu muhimu ya kufikia malengo haya, kwani familia ni msingi wa jamii na inachangia moja kwa moja katika ustawi wa kiuchumi na kijamii.
Kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia 2025, lengo ni kuhamasisha jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti za kuendeleza na kuimarisha sera zinazozingatia familia, ili kufikia malengo haya muhimu ya maendeleo endelevu.