
Rais wa Indonesia, Prabowo Subianto amefanya mabadiliko katika wizara tano, hatua inayoelezwa inalenga kuwatuliza waandamaji.
Taarifa iliyotolewa na kiongozi huyo inasema mabadiliko hayo yamechochewa na wananchi kutoridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kushughulikia masilahi ya waandamanaji wanaoitaka Serikali kuchukua hatua kuhusu matatizo yanayoikabili jamii.
Miongoni mwa mawaziri walioondolewa ni Waziri wa Fedha, Sri Mulyani Indrawati, ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na mkurugenzi mkuu wa Benki ya Dunia.
Vilevile, Budi Gunawan, waziri wa masuala ya siasa na usalama. Wengine ni mawaziri wa vyama vya ushirika, vijana na michezo, na waziri wa ulinzi wa wafanyikazi wahamiaji.
Rais Prabowo amewataka wanaharakati na wananchi kuwa watulivu na kuacha maandamano, akiwaahidi kushughulikia matatizo yanayowakabili.