Mahakama ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mtuhumiwa Richard Peter Mahimbo (25) , Mkazi wa Kiomoni, Tanga, baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.
Mshtakiwa alikamatwa Julai 30, 2025 katika barabara ya Mkinga – Tanga akitumia pikipiki yenye namba za usajili MC 866 EYY, aliyokuwa akiitumia kusafirisha mirungi kutoka Wilaya ya Mkinga kwenda Wilaya ya Tanga Jiji. Mahakama imeamuru pikipiki hiyo kutaifishwa (forfeited) na Serikali.
Akizungumza mahakamani, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Bw. Kelvin Kisanga, aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na vitendo vya kuvunja sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mkinga, Azizi, amesema Mahakama imeridhika pasipo shaka kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa hilo, hivyo kumtia hatiani mtuhumiwa na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela.
Mahakama imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaojihusisha na biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya, ili kulinda usalama na maadili ya jamii.
