
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua mitambo kumi ya uchorongaji na vifaa vya utafiti wa madini yenye thamani wa shilingi bilioni 12.41 kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambayo itapunguza changamoto za wachimbaji wadogo ya kufanya uchimbaji bila kuwa na taarifa za kijiolojia.
Akizungumza baada ya uzinduzi uliofanyika Juni 24, 2025 kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Waziri mkuu Majaliwa amesema kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa juhudi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha shughuli za wachimbaji wadogo wa madini na kuwawezesha kuongeza uzalishaji.
Kadhalika waziri Majaliwa amesema kuwa kuongezeka kwa mitambo ya uchorongaji maalumu kwa wachimbaji wadogo kutaleta mageuzi na manufaa makubwa katika sekta madini. “Moja ya faida kubwa za mitambo hiyo, ni pamoja na kuongeza chachu ya ukuaji wa shughuli za wachimbaji wadogo nchini kwa kuwa itawawezesha upatikanaji wa taarifa za uhakika za jiolojia”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wachimbaji wadogo kuendelea kuuza madini katika viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu ili kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha unaoishia, Sekta ya Madini imefanikiwa kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali kiasi cha shilingi trilioni 1.01.
na kuwa katika miaka miaka minne ya Rais Dkt. Samia madarakani, sekta ya madini imeshuhudiwa ikifanya mapinduzi makubwa ikiwemo kuongeza mchango wake katika pato la taifa ambapo mpaka sasa inachangia asilimia 10.1 kabla ya mwaka wa kimalengo kufika
Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kuamua kuisimamia sekta ya madini ikiwemo kuwawezesha wachimbaji wadogo nchini.