Serikali ya Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera inawasaka watuhumiwa sita, wakiwemo wenyeviti wa vitongoji watatu, kwa tuhuma za kuvamia na kuharibu msitu wa Buyanja uliopo Kijiji cha Businde.
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaitune Msofe, amebainisha kuwa watuhumiwa hao wanatuhumiwa kukata miti ovyo na kuchoma mkaa kinyume na sheria, jambo lililosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira katika eneo hilo.
Afisa Maliasili wa Wilaya, Mektirida Nchimbi, ametoa wito kwa wananchi kuongeza juhudi katika kulinda rasilimali za misitu, huku Diwani wa Kata ya Businde, Gaudin Katabazi, na wakazi wa eneo hilo wakiiomba Serikali kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahujumu hao.
Hatua hiyo inalenga kukomesha tabia ya viongozi wa vijiji kujiingiza katika uharibifu wa mazingira badala ya kuwa walinzi wa rasilimali za umma.
