
Na Shafiru Yusuph- Muleba, Kagera
Halmashuri ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera imerahisisha shughuli za usafiri katika Visiwa 39 vya ziwa Victoria baada ya kununua boti ambayo inauwezo wa kubeba watu 27 yenye gharama ya zaidi ya shilingi milioni 268.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa boti hiyo katika mwalo wa Kyamkwikwi uliopo Kata ya Izigo Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga amesema boti hiyo itahudumia wananchi pamoja na wagonjwa.
Dkt. Nyamahanga amesema kuwa kununuliwa kwa boti hiyo imekuwa msaada mkubwa ikiwemo kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Visiwani na kuwawezesha Viongozi wa Serikali kuwafikia wa urahisi.
Awali akisoma taarifa ya ununuzi wa boti hiyo afisa mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bw. Evart Kagaruki amesema kuwa Wilaya hiyo ilipokea jumla ya shilingi milioni 300 kutoka Serikali kuu ambapo kiasi kilichobaki cha shilingi milioni 31 kitatumika kununua boti ndogo kwa ajili ya doria za Visiwani.