Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari ametoa onyo kali kwa watu au makundi yanayopanga kuandamana, kuleta vurugu au kuzuia wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura akisema kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na vitachukuliwa kama makosa ya jinai.
Johari ametoa onyo hilo leo Jumanne Oktoba 28, 2025, Mtumba Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea kesho Jumatano Oktoba 29 ambapo uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika.
Amesema kuwa katiba ya mwaka 1977 imebainisha wazi kuwa mamlaka yote ya uongozi nchini yanatokana na wananchi, hivyo ni wajibu wa kila raia aliyetimiza umri wa miaka kumi na nane kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa mujibu wa misingi ya demokrasia na utawala bora.
Aidha amebaisha kuwa hakuna sababu yoyote ya kikatiba au kisheria inayoweza kupelekea kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika huku akisema kuwa uchaguzi huo ni halali na unafanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka masharti bayana yanayotaka uchaguzi mkuu kufanyika kila baada ya miaka mitano na huku ikieleza sababu pekee zinazoweza kusababisha kusogezwa mbele kwa uchaguzi ni nchi kuwa vitani au kukosekana kwa wagombea hali ambazo sasa hazipo nchini.