
Baraza la taifa la Watu wanaoishi na virushi vya UKIMWI nchini, NACOPHA wamepongeza serikali kwa kuweka mikakati ya kuendelea kukabilina na VVU pamoja na maambukizi mapya ya virusi hivyo baada ya mabadiliko ya sera za ufadhili kwenye mwitikio wa UKIMWI duniani.
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa NACOPHA Taifa Bi. Leticia Mourice Kapela akiwa mkoani Geita na kueleza kuwa bajeti ya serikali ya mwaka 2025/26 imeonyesha kulishughulikia suala hili ambapo moja ya mkakati ni kufufua viwanda vya kutengeneza dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kikiwemo kiwanda cha Arusha.
Aidha Kapela amesema mwitikio mkubwa unaendelea kuonekana kwa wanaojitokeza kutambua hali za afya zao na wanaotumia dawa na kwamba serikali imefanikiwa kufikia asilimia 90 ya watu wanaotambua afya zao, asilimia 98 wapo kwenye tiba na asilimia 98 wanaendelea kufubaza virusi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu wanaoishi na virusi, NACOPHA Deogratius Rutatwa amewahimiza wanaobainika kuwa na maambukizi kuendelea kuzingatia taratibu za matumizi ya dawa na kuepuka kujinyanyapaa wao wenyewe
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakijinyanyapaa baada ya kupata maambukizi na kusahau kuwa kuishi na maambukizi ya VVU sio dhambi wala sio sifa mbaya, hivyo wanaobainika kuwa na maambukizi waendelee kutumia dawa za ARV ili kudhibiti maambukizi mapya ya virusi hivyo.