
Vijana 199 waliohitimu mafunzo ya Operesheni Nishati Safi katika Kikosi cha 835 Mgambo JKT, wilayani Handeni, mkoani Tanga, wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa busara, hususan wakati huu wa uchaguzi mkuu ili kuepuka taharuki na uvunjifu wa amani.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo Septemba 15, 2025, Brigedia Jenerali Paul Masinde, Kamanda wa Brigedi Makao Makuu Arusha, amesema vijana waliopatiwa mafunzo hayo wameelekezwa kutii sheria na taratibu za nchi, na yeyote atakayekiuka maagizo hayo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kaimu Kamanda wa Kikosi cha 835 Mgambo, Meja Kalist Simon, amewaomba wazazi kuacha mtazamo hasi kuhusu mafunzo ya JKT, akisema yamekuwa chachu ya kuwatengeneza vijana imara, wazalendo na wenye ujasiri.
Baadhi ya wahitimu, akiwemo Veira Munisi na John Nyange, wamesema mafunzo hayo yamewabadilisha kimaadili na kifikra, wakiwajengea ukakamavu, uzalendo na ujasiriamali tofauti na walivyokuwa kabla ya kujiunga.
Mafunzo haya yamewapa vijana uelewa wa jinsi ya kujiepusha na mambo yanayoweza kuharibu amani na familia zao.