
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limethibitisha kupokea taarifa za kuchukuliwa na kurejeshwa kwa mwanamke mmoja aliyejitambulisha Christina Polepole (52), mkazi wa Bahari Beach, Mtaa wa Katumba, Wilaya ya Kinondoni.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo Julai 18, 2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, taarifa kuhusu tukio hilo zilianza kusambaa kupitia mitandao ya kijamii Julai 17, 2025, baada ya Humphrey Polepole ambaye alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba kudai kuwa dada yake alichukuliwa na watu wasiojulikana waliovamia nyumba yao kwa kuruka ukuta.
Kamanda huyo amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa hakuna taarifa zilizokuwa zimewasilishwa mapema kuhusu kutekwa kwa Christina kabla ya kuibuka kwa taarifa hizo mtandaoni.
Aidha, Jeshi hilo limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na wananchi ili kubaini ukweli wa tukio hilo.