
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata na kuwafungia leseni za kuendesha magari madereva 11 kwa kipindi cha miezi mitatu kila mmoja, baada ya kubainika kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, kusababisha ajali na kuharibu miundombinu ya barabara.
Akizungumza na vyombo vya habari Jana, Julai 21, 2025 jijini Mwanza, Kamanda wa Polisi jijini humo, Wilbrod Mutafungwa amesema hatua hiyo ni matokeo ya operesheni maalumu iliyoanza Julai 14, mwaka huu katika barabara zote za mkoa huo kuwakamata madereva wanaofanya matendo yanayohatarisha usalama barabarani.
Amesema operesheni hiyo imekuja baada ya kubaini kuongezeka kwa matukio ya ajali siku za hivi karibuni hususani nyakati za usiku, huku nyingi zikisababishwa na madereva wanaoendekeza pombe, kulewa na kuendesha vyombo vya moto.
Amesema pamoja na hayo, uchunguzi unaendelea na ukikamilika watuhumiwa wote 11 watafikishwa mahakamani.