
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewatoa hofu wananchi kuhusu taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuwa mabaki ya viungo vya binadamu yamekutwa eneo la Magole Mpiji, likisema kuwa taarifa hiyo ni ya zamani na si tukio jipya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 24, 2025 na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo SACP Jumanne Muliro, tukio linalozungumziwa lilitokea mwaka 2014 na lilishachunguzwa kwa kina na mamlaka mbalimbali, huku wahusika kukifikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Polisi wamesema kuwa katika tukio hilo, watu wanne wakiwemo madaktari na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) walikamatwa kufuatia taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu kuwepo kwa viungo vya miili ya binadamu vilivyotupwa katika bonde la Mto Mbezi eneo la Magole Mpiji, Kinondoni.
Uchunguzi uliohusisha Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya na taasisi nyingine za uchunguzi ulibaini kuwa viungo hivyo vilitolewa kwenye maabara ya mafunzo ya IMTU na kutupwa kinyume cha taratibu.
Waliokamatwa walifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mfawidhi wa wakati huo, Kwey Rusema, ambapo Wakili wa Serikali Magoma Mtani aliwasomea mashtaka yanayohusiana na utupaji huo haramu wa mabaki ya miili ya binadamu.
Jeshi la Polisi limeonya kuwa halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaosambaza taarifa za uongo au zenye lengo la kuzusha taharuki miongoni mwa wananchi.