
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amehimiza ushirikiano zaidi na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi baina ya Zanzibar na Japan.
Rais Mwinyi amesema hayo leo Septemba 9, 2025 alipokutana na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Anderson Mutarembwa aliyefika Ikulu mjini Unguja kwa ajili kuaga kabla ya kuelekea katika Kituo chake cha kazi.
Aidha, Dk Mwinyi amempongeza Balozi Mutatembwa kwa uteuzi wake na kumtakia kila la heri pamoja na kumsisitiza kuweka mkazo katika maeneo ya kipaumbele kwa ajili ya ushirikiano na uwekezaji.
Amesema kuwa Japan ina wawekezaji wengi ambao Zanzibar inawakaribisha kuwekeza hususan katika uchumi wa buluu kuangalia namna bora ya kuuza samaki na mazao ya baharini, utalii, michezo, sekta ya mafuta na gesi.
Rais Mwinyi amemueleza Balozi Mutatembwa kuwa eneo jingine ni biashara ya zao la mwani na kumfahamisha kuwa tayari kampuni moja ya Japan imeonesha dhamira ya kuiuzia Zanzibar mtambo wa kuchakata zao hilo na kuliuza nchini humo.
Pia, amesema sekta kuu ya biashara hivi sasa ni uwekezaji katika uchumi wa buluu, na Zanzibar inadhamiria kuwa na viwanda vya kuzalisha bidhaa za baharini, hivyo ni vema kuwavutia wawekezaji zaidi kutoka Japan kuwekeza nchini.
Naye Balozi Mutatembwa amemuhakikishia Rais Mwinyi kuweka mkazo katika utafutaji wa fursa za ushirikiano na kiuchumi nchini Japan, pamoja na miradi zaidi itakayoleta manufaa kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar katika sekta za miundombinu, afya, maji na biashara.