Rais wa Jamuhuri ya Burundi Jen. Évariste Ndayishimiye amewataka vijana wa Afrika kupuuza wanaowashawishi kuingia vitani na badala yake wajikite kwenye miradi ya maendeleo itakayowanufaisha wao na jamii zao.
Rais Gen. Ndayishimiye amesema vijana wengi kupotoshwa na makundi yanayowasukuma kwenye machafuko hukwamisha juhudi za maendeleo barani Afrika kwasababu njia pekee ya kujenga bara lenye ustawi ni vijana kuwekeza katika ubunifu, kazi na uzalishaji.
Kauli hiyo ameitoa katika kongamano la nne la Vijana wa Afrika linalofanyika jijini Bujumbura kwa siku mbili likiwakutanisha vijana kutoka nchi mbalimbali za Afrika kujadili masuala ya vijana, amani, usalama na nafasi yao kwa maendeleo ya Afrika
Kongamano hilo limefanyika chini ya kaulimbiu ya “Vijana Waliojitoa Kuandaa Miradi ya Maendeleo Endelevu, Usindikaji wa Chakula na Madini, Msingi wa Ajenda ya Maendeleo ya Afrika Kupitia Vijana Amani na Usalama”
Lengo kuu la kongamano hilo ni kuwawezesha vijana kubuni miradi ya kimkakati na kuchangia ulinzi wa amani ya mataifa yao.