
Rais Samia Suluhu Hassan, ameshiriki Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika leo, katika Uwanja wa Mashujaa, Mtumba jijini Dodoma.
Maadhimisho hayo ni maalum kwa ajili ya kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwaheshimu mashujaa wote waliotoa maisha, nguvu na sadaka zao kwa ajili ya kulinda uhuru, kudumisha amani na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Katika Maadhimisho hayo Rais Samia ameweka mkuki na ngao katika mnara wa mashujaa ikiwa ni ishara ya kumbukumbu ya mashujaa ambapo pia viongozi wa dini waliomba sala na dua maalum kwa ajili ya kuwaombea mashujaa waliopoteza maisha.
Siku ya Mashujaa huadhimishwa kila mwaka ifikapo Julai 25, ikiwa ni kumbukumbu ya kitaifa ya wale wote waliotoa uhai wao kwa ajili ya kuilinda Tanzania dhidi ya maadui wa ndani na nje, hasa wakati wa harakati za kupigania uhuru na katika operesheni za kulinda mipaka na amani.
Tukio hilo pia linatoa fursa ya kutafakari dhamana ya kizazi cha sasa katika kuendeleza misingi ya uzalendo, uadilifu, umoja na maendeleo ambayo mashujaa wetu walijitoa kuiendeleza.