
Rais Samia Suluhu Hassan leo ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Shule ya Amali Mwamapalala Itilima mkoani Simiyu, akielekeza kuwa lengo la ujenzi wa shule hizo ni kuwafanya wahitimu kuwa na uwezo wa kujitegemea na kuendana na mahitaji ya ajira.
Rais Samia ameweka jiwe la msingi katika shule hiyo kwaniaba ya shule nyingine 26 zinazojengwa Tanzania Bara, amesema Mwelekeo wa serikali ni kukuza zaidi elimu ya amali ili kubadili mwelekeo wa mtoto akimaliza kidato cha nne awe na ujuzi unaomfanya aweze kujiajiri au kuajiriwa.
Katika hotuba yake, Rais Samia amewataka wazazi na walezi mkoani Simiyu kuendelea kutoa fursa za masomo kwa watoto wao ili waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika sekta ya elimu nchini ikiwemo ufunguzi wa matawi ya vyuo vikuu kwenye mikoa mbalimbali na ujenzi wa shule.
Kulingana na Rais Samia, Tangu mwaka 2021 Wilaya ya Itilima imepata shule mpya za msingi 42, za sekondari 31 suala ambalo limeufanya Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kuwa na shule za msingi 606 kutoka 564 zilizokuwepo awali pamoja na sekondari 183 kutoka 152 zilizokuwepo mwaka 2020.