Mgombea urais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewasili jijini Mwanza leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025 kwa ajili ya kufunga mikutano ya kampeni ya chama hicho kesho Jumanne, Oktoba 28, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Katika uwanja wa ndege wa Mwanza, Rais Samia amepokelewa na viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwemo mgombea wake mwenza wa urais, Dk Emmanuel Nchimbi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Asha-Rose Migiro.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kampeni za uchaguzi mkuu zilianza Agosti 28, 2025 na zitahitimishwa kesho Oktoba 28, 2025 na keshokutwa Jumatano ya Oktoba 29 itakuwa ni upigaji kura.
CCM ilizindulia kampeni zake jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Tanganyika Packers na inafunga jijini Mwanza.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu jijini Mwanza amesema mgombea wao wa urais, Samia amefanya mikutano 114 katika mikoa yote nchini.
“Mgombea wetu wa urais amefanya kazi kubwa kunadi ilani ya CCM hadi sasa, tuna uhakika Watanzania wameielewa na wako tayari kuichagua CCM kwa sababu uchaguzi wa 2025 tumekuwa na ilani bora ya uchaguzi kuliko zingine, CCM ndiyo imebeba matumaini ya Watanzania,” amesema Kihongosi.
