
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeingia mkataba na mkandarasi mzawa, kampuni ya Samota Ltd, kwa ajili ya kujenga mradi wa skimu ya umwagiliaji Mwamapuli, uliopo katika Kijiji cha Mwanzugi, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, kwa gharama ya shilingi bilioni 26.9.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha kazi inafanyika kwa ufanisi na ndani ya muda wa mkataba kama walivyokubaliana na Serikali.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Tabora, Francis Mgangalula, amesema utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa barabara za mashambani, ofisi ya Tume, nyumba ya meneja wa skimu pamoja na ununuzi wa gari moja kwa ajili ya usimamizi wa mradi.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka kampuni ya Samota Ltd, Ahmed Salumu, ameahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati na kwa viwango vya ubora vinavyotakiwa, kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 720, ukilenga kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 630 hadi kufikia hekta 2,397, ambapo zaidi ya wakulima 2,470 wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja na huduma ya umwagiliaji kutoka skimu hiyo.