Uongozi wa Singida Black Stars umetangaza kumuondolea adhabu ya kusimamishwa kiungo wao Khalid Aucho baada ya kupitia kwa kina maelezo yake pamoja na barua ya kuomba radhi aliyoiwasilisha kufuatia kosa lililomkabili.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na klabu hiyo Machi 5, 2026, Kamati ya Nidhamu ya Singida Black Stars ilikaa na kujadili suala hilo baada ya kukamilika kwa uchunguzi pamoja na maelezo kutoka kwa mchezaji huyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa awali Aucho alikuwa amepewa adhabu ya kusimamishwa kwa miezi mitatu, lakini kutokana na majuto na dhamira aliyoionesha, uongozi umeamua kumuondolea adhabu hiyo na kumruhusu kurejea kikosini kuendelea kuitumikia timu.
Klabu hiyo imeeleza kuwa itaendelea kusisitiza nidhamu, uwajibikaji na weledi kwa watumishi wake wote kama sehemu ya kuhakikisha timu inaendeshwa kwa misingi ya taaluma na heshima ndani na nje ya uwanja.
