Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa kushirikiana na Taasisi ya Global Education Link Ltd wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kukuza tafiti, ubunifu na maendeleo ya kisayansi.
Makubaliano hayo yatasaidia kuandaa kizazi kipya kitakacholeta mapinduzi ya kiuchumi na kiteknolojia Barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Ushirikiano huo unatarajiwa kufungua milango ya fursa mpya katika sekta ya elimu, utafiti na ubunifu, pamoja na kuitangaza taasisi hiyo kimataifa ili dunia itambue kuwa Tanzania ina taasisi inayozalisha vipaji na teknolojia za kisasa kupitia ushirikiano na vyuo vikuu mbalimbali vya nje ya nchi.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Makamu Mkuu wa Taasisi ya Nelson Mandela, Profesa Maulilio Kipanyula, amesema Afrika ina hazina kubwa ya vipaji ambavyo vikisimamiwa na kupangwa vizuri vinaweza kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Global Education Link Ltd, Abdullmalik Mollel, amesema ushirikiano huo umejikita katika kuimarisha masuala ya kitaaluma, uwekezaji na matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija katika sekta ya elimu na uchumi.
Anasema elimu inayotolewa kwa wanafunzi inapaswa kuwa na mchango wa moja kwa moja katika kukuza uchumi na maendeleo kwa kutumia teknolojia, maarifa na mitaji.

Kwenye picha ni Makamu Mkuu wa Taasisi ya Nelson Mandela, Profesa Maulilio Kipanyula, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Global Education Link Ltd, Abdullmalik Mollel,
Makubaliano hayo ni mwanzo wa safari ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi hizo mbili, wenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa vyuo vikuu na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu, utafiti na maendeleo ya jamii kwa ujumla
Elimu anayopewa mwanafunzi inapaswa kusaidia kukuza uchumi na kuleta maendeleo kupitia teknolojia, maarifa na uwekezaji. Ushirikiano wa maarifa kati ya vyuo vikuu mbalimbali utaongeza tija katika kukuza uchumi unaotegemea teknolojia
