
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Japan, Ishiba Shigeru ambaye amemuhakikishia kuwa nchi hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania ili kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na fursa zitakazoendelea kupatikana kupitia ushirikiano huo.
Wakati wa mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Mei 29, 2025 katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Japan Jijini Tokyo, Majaliwa amesema ahadi hiyo inazidi kutoa fursa kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kumueleza Waziri Mkuu huyo wa Japan kuwa pamoja na miradi mingine wanayotekeleza Tanzania kupitia JICA, iangalie uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara za Morogoro-Dodoma na barabara ya Kibiti-Lindi iliyoharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Waziri Mkuu wa Japan baada ya kupata maelezo hayo ameuelekeza uongozi wa JICA pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Youichi Mikami kwenda kutembelea barabara hizo na kuzifanyia tathmini ya uharibifu na kisha kuwasilisha taarifa ili Serikali ya Japan ione namna itakavyoshirikiana na Tanzania katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amepongeza kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan, na kuahidi kuhakikisha kampuni mbalimbali za Japan zinaendelea kufanyakazi na Tanzania ili kuisaidia katika kukuza uchumi, kuendeleza masuala ya kijamii na teknolojia kwani wanatambua idadi ya watu Tanzania inaendelea kuongezeka.