
Serikali ya Tanzania imesema kuna umuhimu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani ili kujenga uelewa kuwa, zoezi la uimarishaji wa mpaka kati ya Tanzania na Rwanda, halilengi kutenganisha jamii hizo bali ni daraja la kujenga mahusiano mazuri.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Ngara mkoani Kagera Kanali Mathias Kahabi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, wakati wa mkutano wa wataalam wa kamati ya ufundi ya pamoja kutoka nchi za Tanzania na Rwanda uliofanyika Wilayani Ngara.
Kanali Kahabi amesema serikali ya Tanzania iko tayari kutoa mahitaji yote ikiwemo rasilimali fedha ili kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa ajili ya kukamilisha zoezi la uimarishaji wa mipaka baina ya nchi hizo mbili.
Naye Mkuu wa utafiti kutoka nchini Rwanda na kiongozi wa timu ya wataalam kutoka Rwanda Abeli Mahungu amesema kikao hicho cha siku tano kinalenga kuhakikisha mchakato huo unatekelezwa kwa mafanikio ili kujenga mahusiano ya ndani kati ya Tanzania na Rwanda.