Benki ya Maendeleo TIB kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wamesaini Hati ya Makubaliano (MoU) yenye lengo la kuendeleza mifumo bunifu ya ufadhili wa maendeleo na kuchochea mageuzi ya kijamii na kiuchumi nchini.
Ushirikiano huo unalenga kufungua fursa za uwekezaji katika sekta za kimkakati ikiwemo nishati jadidifu, biashara ndogo na za kati (SMEs), uchumi wa buluu pamoja na miradi ya vijana.
Pia utawezesha utambuzi na uendelezaji wa miradi yenye mvuto kwa wawekezaji kupitia mifumo ya ufadhili mseto (blended finance) na kuongeza utayari wa uwekezaji.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Deogratius Kwiyukwa, amesema ubia huo unaakisi dhamira ya pamoja ya kuharakisha maendeleo endelevu kwa kutoa mitaji ya muda mrefu na suluhisho bunifu za kifedha kwa sekta muhimu za uchumi.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Shigeki Komatsubara, alieleza kuwa ushirikiano na taasisi za kifedha za ndani ni muhimu katika kuongeza athari za maendeleo, huku ukilenga kukuza uchumi jumuishi, kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi na kupanua fursa kwa jamii.
Makubaliano hayo yanaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuharakisha mageuzi ya uchumi, kukuza uwekezaji na kulinda mazingira.
Ubia huo pia utaimarisha uwezo wa taasisi, kukuza ujasiriamali, kuzalisha ajira hasa kwa Vijana na kuharakisha utekelezaji wa miradi yenye matokeo chanya kwa uchumi wa Tanzania.
