Anaandika Padre Tobias Dindi Ong’aria wa Shirika la Yesu ambaye alijikuta amebaki yeye na jeneza.
“Hii ni simulizi ambayo nimekuwa nikitaka kuisimulia kwa muda mrefu, lakini nimekuwa nikishindwa kuipanga vizuri.
Nilipowekwa wakfu kuwa padre mwezi Julai 2023, nilirudi Paris ambako nilikuwa nimetumia mwaka mmoja nikisoma Falsafa katika mazingira ya kitamaduni yaliyokuwa tofauti sana na yale niliyozoea.
Moja ya nyakati zilizonifanya nijisikie tofauti kiutamaduni ilitokea tarehe 27 Mei 2024. Nilikuwa naishi katika jumuiya ya Wajesuiti ndani ya Jimbo Katoliki la Saint Denis.
Nilipokea ombi kutoka kwa katibu wa jimbo la kanisa ili nikaongoze ibada ya mazishi ya mwanaume mmoja aliyefariki siku chache kabla, jina lake Marcel.
Nilipewa mawasiliano ya mke wake na binti yake, nikawasiliana nao ili tuweze kuandaa ibada pamoja. Tulizungumza, tukapanga muundo wa ibada, na tukakubaliana kukutana kwenye kanisa lililopo ndani ya makaburi.
Makaburi ya huko ni tofauti sana na nilikotoka, yamepangwa vizuri, yamejengwa kwa utaratibu, na yana uzuri na utulivu wa pekee.
Eneo hilo lilikuwa makaburi ya Joncherelles huko Saint Denis, Paris. Kuna makanisa madogo ambapo familia hukusanyika, huomba, na kutoa heshima za mwisho kabla ya mazishi au uchomaji wa mwili.
Kila kitu kilikuwa kimepangwa. Nilichukua treni majira ya saa tano asubuhi, lakini kwa bahati mbaya ndugu na familia hawakutokea. Hakukuwa na maelezo yoyote hawakuweza tu kufika.
Nilipofika mapokezi, nilijitambulisha: “Bonjour, je suis le Père Tobias, je suis venue pour célébrer les funérailles de Marcel.” (Yaani: Habari, mimi ni Padre Tobias, nimekuja kuongoza ibada ya mazishi ya Marcel)
Nikaambiwa: “Allez à la chapelle numéro 5” (Nenda kwenye kanisa namba 5)

Nilipofika kwenye kanisa namba 5, hapo ndipo nilijikuta nimesimama ndani ya kanisa hilo, na mbele yangu kulikuwa na mwili wa marehemu ukiwa kwenye jeneza.
Tulikuwa wawili tu. Niliendesha ibada yote ya mazishi nikiwa peke yangu. Ndipo nikajikuta najiuliza, inawezekanaje mtu akawa peke yake kiasi hiki?
Leo, katika Ijumaa Kuu, swali hilo linakuwa zito zaidi. Kwa sababu kiini cha siku hii pia kinahusu upweke wa aina fulani.
Kristo, aliyeachwa, aliyesalitiwa, aliyekataliwa, na kuachwa akabiliane na kifo kana kwamba yuko peke yake kabisa. Hata wale waliokuwa karibu naye hawakuweza kubaki naye. Hata waliompenda walishindwa kusimama imara.
Kuna kitu kinachotutia hofu ndani ya upweke wa kifo. Unatukumbusha ukweli ambao mara nyingi tunauepuka: Kwamba mahusiano yanaweza kushindwa, Uwepo wa watu si jambo la uhakika na mwishowe, hatuwezi kudhibiti nani atakuwa nasi.
Na bado, Ijumaa Kuu inafunua jambo lingine kwamba upweke si neno la mwisho, hata katika kuachwa, kuna uwepo uliojificha, hata katika ukimya, kuna ushirika wa ndani zaidi, hata katika kifo, kuna fumbo linaloendelea ambalo hatulioni kikamilifu.
Siku ile kanisani, ilionekana kana kwamba yule mtu alikuwa peke yake kabisa. Je ni kweli alikuwa peke yake? Au kulikuwa na uwepo mkubwa zaidi ya kutokuwepo kwa wanadamu?
Ijumaa Kuu inatualika si tu kuomboleza kifo, bali pia kutafakari namna tunavyoishi, Tunajitokeza kwa ajili ya nani? Ni nani anayebeba upweke kimya kimya hata sasa? Na ina maana gani kubaki pamoja na mtu, hata pale inapokuwa vigumu, haieleweki, au inatuhitaji kujitoa zaidi?
Kwa sababu wakati mwingine, tendo kubwa zaidi la upendo ni hili tu KUWEPO.
Na pale tunaposhindwa kwa sababu sisi ni binadamu Ijumaa Kuu inatukumbusha kwamba Mungu hashindwi kamwe. Hata katika nyakati za upweke mkubwa, hakuna mtu aliye peke yake kweli.
Neema za Kristo aliyesulubiwa zikuhakikishie amani.”
Umejifunza nini katika TAFAKARI YA IJUMAA KUU ya leo Aprili 02, 2026?
