
Tanzania na Rwanda zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo, baada ya kukamilika kwa kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu (JTC) kati ya nchi hizo mbili kilichofanyika Ngara Mkoa wa Kagera.
Utiaji saini makubaliano hayo umefanyika Juni 12, 2025 kati ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour kwa upande wa Tanzania na Abel Buhungu ambaye ni kiongozi wa ujumbe kutoka Rwanda.
Akizungunza mara baada ya kusaini makubaliano hayo Mansour amepongeza hatua iliyofikiwa ya kutiwa saini makubaliano ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Rwanda na kueleza kuwa ni matumaini yake maazimio yaliyofikiwa yatatekelezwa kama walivyokubaliana.
Naye kiongozi wa ujumbe wa Rwanda ambaye ni Mkuu wa Ubalozi wa Rwanda nchini Sudan, Abel Buhungu ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuialika nchi yake kushiriki kikao cha pamoja cha uimarishaji mpaka wa kimataifa kwa nchi hizo mbili na kuongeza kuwa hana wasiwasi kwa kazi iliyofanyika na muda si mrefu watafikia malengo yaliyokusudiwa.
Wakati wa kikao cha JTC wajumbe walipata fursa ya kukagua mpaka wa kimataifa wa Tanzania na Rwanda ambapo ukaguzi ulianzia katika alama ya mpaka ya Mafiga Matatu (Kasange) mahali ambapo mto Kagera unakutana na mto Mwidu kisha kuelekea Rusumo mahali ambapo mto kagera unakutana na mto Ruvubu.
Lengo la ukaguzi wa mpaka ni kubaini hali halisi ya mpaka ulivyo, maendelezo yanayoyafanyika na yale yaliyofanyika pamoja na shughuli za kibinadamu zinazofanyika.
Mpaka wa Tanzania na Rwanda una urefu wa takriban km 230.
Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya umoja wa Afrika kuwa ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.