
Ujenzi wa Barabara ya Buhongwa-Igoma yenye urefu wa Km 14 kwa kiwango cha lami inayojengwa katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza inatajwa kuwa ndio mwarobaini wa changamoto ya msongamano wa magari jijini humo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Wakili Kiomoni Kibamba wakati akielezea hali ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Jiji la Mwanza kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji na Majiji Tanzania (TACTIC) na manufaa yake kwa wananchi.
Amesema barabara hiyo inayounganisha Kata nne ambazo ni Buhongwa, Lwanhima, Kishiri na Igoma ilikuwa na changamoto kubwa hali iliyopelekea magari yote yaliyokuwa yakitoka Buhongwa kwenda Igoma au Igoma kwenda Buhongwa kulazimika kuingia katikati ya jiji hivyo kuongeza msongamano wa magari.
Hata hivyo baadhi ya wananchi kwa upande wao wamesema yafuatayo Bw. Kalumanzila Idd, Mkazi wa Buhongwa, jijini Mwanza ameishukuru serikali kwa kuwajengea barabara hiyo kwani imewaondolea adha ya usafiri iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu.
Pia Judith S. Maningo Mkazi wa Mtaa wa Ihushi, Kata ya Kishiri amesema kuwa pamoja na Rais Samia kuwapelekea Miradi mingi ya maendeleo lakini ujenzi wa barabara ya Buhongwa-Igoma umeleta ukombozi mkubwa kwa wana Ihushi na Kishiri kwa ujumla