Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, ambapo kiwango cha upatikanaji kimefikia asilimia 88.8 mwezi Februari 2026, kikilinganishwa na wastani wa asilimia 73 mwaka 2021/22.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa, Machi 10, 2026 wakati akiwasilisha hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa nyingine za afya mbele ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azzan Zungu na Kamati ya Kudumu ya Bunge la Afya na Masuala ya Ukimwi, katika ukumbi mdogo wa Bunge, jijini Dodoma.
“Taarifa inaonesha kuwa upatikanaji wa bidhaa 382 za kipaumbele zenye shehena inayotosheleza zaidi ya mwezi mmoja umeongezeka kutoka asilimia 49 mwaka 2021/22 hadi asilimia 73 mwaka 2025/26, aidha, bidhaa zenye akiba ya zaidi ya miezi minne zimeongezeka kutoka asilimia 25 hadi asilimia 40,” amesema Mchengerwa.

Ameeleza kuwa wastani wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya umeongezeka kutoka asilimia 73 mwaka 2021/22 hadi asilimia 88.8 mwezi Februari 2026 huku Hospitali za Taifa, Maalum na Kanda zimefikia asilimia 97.68.
“Hospitali za rufaa za mikoa zimefikia asilimia 95.93, Hospitali za Wilaya asilimia 83.81, Vituo vya afya asilimia 82.83, na Zahanati asilimia 79.46,” amesema.
