
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema uhusiano mzuri wa kidiplomasia na ushirikiano wa maendeleo baina ya Tanzania na Canada umeendelea kuipaisha sekta ya afya nchini.
Waziri Mhagama amebainisha hayo Julai 20, 2025 mara baada ya kumpokea Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Randeep Sarai pamoja na ujumbe alioambatana nao kutoka nchini Canada waliowasili kwa lengo la kufanya ziara ya siku tano (5) nchini.
Aidha Waziri Mhagama ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Canada kwa kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo ya sekta ya afya nchini Tanzania, kwa mchango wanaoutoa kwenye mfuko wa pamoja wa afya (Health Basket Fund) ambao unasaidia katika uboreshaji wa huduma za afya ngazi ya msingi kupitia mfumo wa ufadhili wa moja kwa moja katika vituo vya afya awamu ya kwanza (2022–2027).
Sanjari na hayo amebainisha kuwa Tanzania imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Canada katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, haki za vijana balehe pamoja na kuimarisha huduma za uuguzi wakati wa kujifungua ambazo zinalenga kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga kwa kuongeza upatikanaji wa wakunga wenye ujuzi.
Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Canada katika sekta ya afya umeleta mafanikio mengi ikiwemo kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 67 mwaka 2015 hadi asilimia 43 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 1,000, kupungua kwa vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai laki 100,000
Pia Waziri Mhagama ameelezea changamoto ya kasi ndogo ya kupungua kwa vifo vya watoto wachanga, kutoka vifo 25 kwa kila vizazi hai elfu 1,000 mwaka 2015 hadi vifo 24 kwa kila vizazi hai elfu 1,000 mwaka 2022 na kutumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Canada kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza afua za afya zinazolenga kutatua changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Randeep Sarai ameshukuru kwa mapokezi mazuri nchini Tanzania na ameahidi nchi hiyo kuendelea kutoa ushirikiano hasa katika sekta ya afya.