
Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeahidi kuanzisha mamlaka mpya ya kusimamia mazao yote ya kimkakati likiwemo la kahawa, kwa lengo la kuondoa changamoto sugu zinazowakumba wakulima hasa wa Mkoa wa Kagera.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Mshabago, wilayani Muleba, mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chaumma, Salum Mwalimu amesema serikali yake itakapochaguliwa Oktoba 29, 2025, itahakikisha kunakuwepo na usimamizi madhubuti wa sekta ya kilimo kwa kuvunja bodi zote ambazo hazitekelezi majukumu yake ipasavyo.
Amesema mamlaka hiyo mpya itakuwa na jukumu la kupandisha bei ya kahawa kwa kuweka mazingira ya ushindani wa soko huria, huku akisisitiza kuwa utumishi wa mamlaka hiyo utakuwa wa uwajibikaji wa hali ya juu, watendaji wake watapimwa kila mwezi na malipo yao kutegemea ufanisi wao na mwenendo wa soko.
Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chaumma, John Mrema amesema kuwa wakulima wa Kagera wamekuwa wakinyanyaswa na kunyimwa fursa ya kuuza kahawa yao kwenye masoko huru, tofauti na ilivyo kwa wakulima wa maeneo mengine kama Kilimanjaro.
Mrema amewataka wananchi kuachana na chama tawala akidai kimeshindwa kuwaletea maendeleo na haki za msingi za kiuchumi, hivyo ni wakati wa kuonyesha hasira zao kwa kutumia sanduku la kura.